TASAF na washirika wa maendeleo wanaofadhili Mpango wa kunusuru Kaya Masikini na zinazoishi katika mazingira hatarishi watembelea kisiwani Zanzibar

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 Mkuu wa Mkoa wa Kusimni Unguja.Dkt. Idris Muslim Hijja, akizungumza na Ujumbe wa Tasaf  na Wawakilishi wa kutoka Nchi Wafadhi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini PSSN  kabla ya kutembelea Shehia ya Kikungwi.
  Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF mwenye suti nyeusi Ndg. Ladisilaus Mwamanga, akizungumza katika  Ofisi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt Idris Muslim Hijja, kabla ya kuaza kwa ziara hiyo.
 Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bi. Ida Manjoro, akizungumza wakati walipofika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja kujitambulisha kwake kabla ya kuanza kwa ziara yao kutembelea Kaya Masikini Unguja.
 Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ndg. Ladisilaus Mwamanga, akizungumza na Walengwa wa Kaya Maskini katika shehia ya Kikungwi Unguja. 
 Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini  katika shehia ya Kikungwi Wilaya yaKati Unguja wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf akizungumza katika mkutano huo.

 Picha ya pamoja

=======  =====  =======
Ujumbe kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF na washirika wa maendeleo wanaofadhili Mpango wa kunusuru Kaya Masikini na zinazoishi katika mazingira hatarishi uko kisiwani Zanzibar kuona namna Mpango huo unavyotekelezwa kisiwani humo. Ujumbe huo umepata fursa ya kutembelea shehia ya Kijini Matemwe mkoa wa Kaskazini Unguja na Shehia ya Kikungwi wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja ambako umezungumza na walengwa wa  mpango huo.

Wakizungumza na viongozi hao baadhi ya walengwa wameonyesha kuridhika na mpango wa kunusuru kaya masikini ambapo wamesema maisha ya kaya hizo yameanza kuboreshwa huku mmoja wa walimu wa shule ya msingi Kikungwi Amrani Kombo akibainisha kuwa tangu kuanza kwa Mpango huo  mwaka jana kumekuwa na mahudhurio mazuri kwa wanafunzi kutoka katika kaya masikini ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kuanza kwa mpango huo.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bwana Ladislaus Mwamanga amesema Mpango huo umeanza kutekelezwa kwa awamu nchini baada ya serikali kuridhia utekelezaji wake katika jitihada za kupambana na umasikini miongoni mwa wananchi. Amesema  utafiti umefanywa kwa kina kuona namna ya kuutekeleza mpango huo ili uweze kuleta mabadiliko chanya katika ya maisha  ya wananchi wanajumuishwa katika mpango huo.

Dkt. Shein Azungumza na Uongozi Wizara ya Miundombinu Mawasiliano

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akizungumza na Uongozi wa Wizara Miundimbinu na Mawasiliano katika Utekelezaji wa Mpango kazi wa robo mwaka kutoka Julai-Machi 2013/2014,ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Unguja leo asubuhi.
[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

MAALIM SEIF ASHAMBULIWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Adaiwa kuiba waraka
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Maalim Seif Sharif Hamad
 
Utetezi wa muundo wa Muungano wa serikali mbili katika mjadala wa katiba jana ulichukua sura mpya kwa kuelekeza mashambulizi mengi dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif  Hamad kuwa ni mtu kigeugeua sawa na kinyonga.
Mashambulizi hayo yalianza asubuhi wakati Mohammed Seif Khatib alijadili sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya katiba, akimwelezea Maalim Seif kuwa ni mtu anayebadilika kama kinyonga, kiasi cha kudirikia kuiba nyaraka Ikulu iliku kuulinda Muungano wa serikali mbili, lakini sasa amegeuka na kusaka serikali tatu na Muungano wa mkataba.

Khatib alisema kuwa Maalim Seif aliwachongea viongozi wa Zanzibar, akiwamo Rais wa awamu ya pili, Abood Jumbe, ili kutetea Muungano wa serikali mbili.

Mbali na Jumbe, wengine wanaodaiwa kuchongewa na Maalim Seif mwaka 1984, ni Waziri Kiongozi mstaafu, Ramadhani Haji Fakhi, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wolfgang Dourado, wa wakati huo.

Alisema Maalim Seif aliwashitaki viongozi hao kwa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye mkutano wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho mwaka huo akidai kwamba walitaka kubadilisha katiba na kuwa na Muungano wa serikali tatu.

Khatib alisema Maalim Seif alidai kuwa Dourado alikuwa anasafiri kati ya London na Zanzibar ili kukashifu viongozi wa Muungano na kuwachochea watu wauchukie kuwa siyo wa halali.

 Alisema Maalim Seif alidai kuwa kwa safari hizo Dourado aliangamiza fedha za kigeni na kuhoji alipata wapi jeuri ya kuwasemea Wazanzibari.

Khatib alimnukuu Maalim Seif akisema kuwa viongozi hao walifanya vitendo vya uhaini na kutaka Halmashauri Kuu (Nec) iwahukumu.

Alinukuu kauli za Maalim Seif aliyesema: “Suala la serikali tatu limepewa uzito mkubwa katika waraka na linachochewa na Makamu Jumbe.”

Aidha, alimtuhumu Maalim Seif kuwa ni kiongozi wa ajabu aliyediriki kuiba waraka wa siri kwenye Ikulu ya Zanzibar na kuungama kuwa alifanya hivyo kama alivyonukuliwa kwenye kitabu cha Profesa Issa Shivji.

Khatib alisema Maalim Seif aliiba waraka huo kwenye shubaka (droo) ya Rais Ikulu ili kutetea muundo wa serikali mbili.

Alimfananisha Maalim Seif na kinyonga, ambaye mwaka 1984 alitetea serikali mbili baada ya kutimuliwa CCM Mei 13, 1988, alitaka serikali tatu na mwaka jana akaibuka na Muungano wa mkataba.

DK. MWAKYEMBE AONGEZA MASHAMBULIZI
Dk. Harrison Mwakyembe naye aliendeleza mashambulizi dhidi ya Maalim Seif alipomkariri katika moja ya hotuba zake akisema:

 “Naamini maslahi ya Zanzibar yana uhakika zaidi katika Muungano huu, ambao umesaidia kuzuia machafuko na kuepusha vifo vya watu wasio na hatia Zanzibar na kwamba, ndiyo uliodumisha amani.”

Alimnukuu akiahidi: “Nitaandelea kudumisha Muungano na kuyatetea maslahi ya Zanzibar.”

Dk. Mwakyembe alisema Maalim Seif licha ya kuteta serikali mbili katika mfumo wa Muungano, aliwahi kudai kuwa kero zilizoko siyo za msingi.

Naye Hamad Rashid Mohammed alitumia fursa ya jana kuweka wazi walivyohusika yeye na Maalim Seif kupeleka waraka wa Jume kwa Mwalimu Nyerere baada ya kuongea na Waziri Mkuu, Edward Sokoine.

Hamad alisema kuwa walimfuata Mwalimu Butiama baada ya kusoma waraka wa Jumbe, aliitisha kikao cha Kamati Kuu lakini mwafaka haukupatikana ikabidi Nec iitishwe na mwishowe maamuzi ya kuvuliwa madaraka Jumbe yalifikiwa.

Alisema kuwa Ali Hassan Mwinyi aliagizwa kugombea urais Zanzibar na alitakiwa amteue Maalim Seif kuwa Waziri Kiongozi.

Alimshutumua Maalim Seif kwa usaliti na kwamba anajitwisha Uzanzibari kuliko Wazanzibari wengine, lakini kinachomsumbua ni kutaka madaraka tu kwani alimfaia vitimbi pia Mzee Abdul Wakili, ambaye akiteuliwa kugombea urais baada ya Mwinyi kuwa Rais wa Tanzania.
CHANZO: NIPASHE

Jumuiya ya KOKNI Jamat ya Zanzibar yashinda Bonanza la Pasaka dhidi ya wenyeji wao wa Bara

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
DSC_2095
Wachezaji wa Timu ya Kokni Jamat ya Zanzibar wakiteremka kwenye boti wakitokea Dar es laam kwenye Bonanza la Pasaka ambapo wamefanikiwa kuchukuwa makombe  matatu ya mshindi wa kwanza katika michezo ya Play Station,  mpira wa meza na mpira wa miguu dhidi ya wenyeji wao. Aliebeba kombe kubwa ni Rais wa Jumuia ya Kokn Jamat ya Zanzibar Jeff Babu.
DSC_2122
Wachezaji wa Timu ya Kokni Jamat ya Zanzibar katika picha ya pamoja. 
DSC_2149
Nahodha wa Timu ya Kokni Jamat Ibrahim Dalvi (kulia) na msaidizi wake Nabil Shamshuddin wakiwa wameshikilia kombe mara baada ya kuwasili Zanzibar.(PICHA NA MAKAME MSHENGA-MAELEZO ZANZIBAR).

'VURUGU BUNGENI CHANZO NI PROPAGANDA'

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba
 
Emeelezwa kuwa vurugu zinazoendelea katika Bunge Maalumu la Katiba zinatokana na propaganda za wanasiasa wanaopigania maslahi yao binafsi  za kuwalisha maneno Wazanzibari kwamba msimamo wao ni serikali tatu .
Akizungumza na waandishi wa habari,mmoja wa viongozi kutoka Zanzibar, Msim Seifu Abdallah, alisema bunge hilo linayumbishwa na baadhi ya wajumbe wake ambao hawana uzalendo na utaifa na badala yake niwapigania maslahi binafsi.

Msim  ambaye ni Diwani wa ya Mfenisini Wilaya ya Magharibi Zanzibar, alisema kuwa baadhi ya wanasiasa ndani ya bunge hilo ni wapiga propaganda na kuwalisha maneno Wazanzibari kuwa wanataka serikali tatu.

Alidai kuwa msimamo wa Wazanzibari ni serikali mbili na siyo tatu kama wanavyosimamia baadhi ya wajumbe wa bunge hilo.

“Wazanzibar bado tunawaenze waasisi wa iliyokuwa Tanganyika, Hayati Mwalimu Nyerere na Zanzibar, Hayati Karume, wao walisimamia serikali mbili……sisi hatuwezi kuwa tofauti na wao, vinginevyo ni propaganda za wanasiasa kutuopakazia maneno ya serikali tatu,” alisema Msim.

Hata hivyo, Msim aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kufikilia Tanzania kwanza na kwamba wasitumie nafasi hiyo kwa malumbano kutumika wala maslahi yao binafsi,kikundi au mtu.             

Katika hatua nyingine, Msim  aliwataka Watanzania bara na Wazanzibar kutosikia  maneno  yanayokienezwa  kuhusu msimamo wa Wazanzibari kuwa ni serikali tatu kwani ni ya uongo na propaganda za wanasiasa
CHANZO: NIPASHE

KAULI YA INTERAHAMWE YAMCHEFUA ASKOFU MTETEMELA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Askofu Donald Mtetelela (pichani), ameeleza kusikitishwa kwake na Bunge hilo kuitwa Interahamwe.
Akizungumza bungeni jana, Askofu Mtetemela, ambaye ni Mkuu wa Kanisa la Anglikana mstaafu, alisema alishangazwa na kauli hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye anaheshimika kimataifa.

Profesa Lipumba juzi jioni alililinganisha bunge  hilona kundi la interahamwe lililochochea ubaguzi wa kikabila uliosababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda kutokana na kukumbatia na propaganda.

Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo iliyosababisha wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje, akidai kuwa kauli alizozitoa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Jumamosi iliyopita ni za ubaguzi.

Lukuvi akizungumza katika sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Kanisa la Methodist Dodoma, alisema mfumo wa serikali tatu haufai na kwamba serikali ya Muungano ikikosa mapato itasababisha wanajeshi kukosa mishahara na kuiangusha serikali.

Lukuvi pia alisema kwamba kuruhusu  serikali tatu kutasababisha kuibuka kwa siasa kali za Kiislamu upande wa Zanzibar na kuishutumu CUF kuwa inatekeleza siasa za kidini za kikundi cha Uamsho.

Askofu Mtemele alisema kauli ya Prof. Lipumba kuliita bunge hilo kuwa ni Interahamwe hakuwatendea haki wajumbe na kwamba alitaka amuone azungumze naye, lakini ametoka nje na wajumbe wenzake.

“Kutuita Interahamwe ni ubaguzi, Interahamwe ni kundi la wauaji, kutuita sisi ni wauaji siyo nia njema na inaweza kufufua hisia za wananchi wa Rwanda na serikali ya Rwanda kwamba tunatumia Interahamwe,” alisema Askofu Mtetemela. Alihoji: “Kwa nini tuinue suala hili tena linaloibuliwa na kiongozi kama yeye (Lipumba) anayeheshimiwa kimataifa?

Askofu Mtetemela alisema kuwa haikuwa busara kuibua suala hilo kwa kuwa Tanzania na Rwanda zilikuwa na tofauti katika siku za karibuni, hivyo kauli hiyo inaweza kuzorotesha uhusiano baina ya nchi hizo.

Askofu Mtetemela pia alisema siyo busara kuwakashifu waasisi wa Muungano ambao alisema ndiyo walioweka msingi wa utulivu na amani nchini.

Alisema ujenzi wa katiba ni maridhiano. Tuzungumze na tusikilizane, tushauriane na ikiwa kuna jambo tulimalize,” alisema.

“Vyama vyetu vitutajirishe na siyo kutubomoa,” alisema na kuongeza: “Tunapaswa kuangalie yasiyo sahihi ili yarekebishwe.”
SOURCE: NIPASHE

RAIS DK.SHEIN AKIZUNGUMZA NA UONGOZI WA WIZARA KATIBA NA SHERIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
IMG_9916Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein  (kulia) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria,katika kikao cha utekelezaji Mpango kazi kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini  Zanzibar jana jioni, [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
IMG_9926Baadhi ya Viongozi wa Wizara ya  Katiba na Sheria wakiwa katika kikao cha utekelezaji wa mpamgo wa kazi kwa kipindi cha robo mwaka kutoka Julai -Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Zanzibar jana jioni, chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
IMG_9930
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein  (kushoto) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria,katika kikao cha utekelezaji Mpango kazi kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini  Zanzibar jana jioni, [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

ZANZIBAR ISAIDIWE KUBORESHA HUDUMA ZA KIFEDHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Zanzibar ndiyo mkoa wa kwanza wenye idadi ndogo ya watu wanaopata huduma za kifedha, licha ya kuwa na mitandao ya simu kama ile iliyopo bara.
Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT) inaonyesha kuwa Zanzibar inashika mkia licha ya Tanzania kuongoza duniani kwa kutumia simu kujipatia huduma za kifedha.
Idadi ya wanaotumia benki imeongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2009 mpaka asilimia 13.9 mwaka 2013.
Aidha, asilimia 73.2 ya watu hao wamekuwa wakipata huduma za kifedha zinazojumuisha bima, vyama vya kuweka na kukopa na kutuma na kupokea fedha kupitia taasisi nyingine mbalimbali zilizoanzisha huduma za kutoa huduma za fedha.
Ongezeko hili la wanaopata huduma hizi linaonekana zaidi kwa watu wa bara pekee kwani, kwa Zanzibar, takriban asilimia 50 hawapati huduma hizi.
Huko, asilimia 11.5 ya watu wamekuwa wakitumia benki wakati asilimia 25.5 wamekuwa wakipata huduma hizo kupitia simu na asilimia 17.1 wanatumia huduma nyinginezo za fedha.
Hali ni tofauti na Mkoa wa Kilimanjaro unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wapatao huduma za kifedha ikifuatiwa na Dar es Salaam.
Mkoa wa Kilimanjaro una asilimia 93.8 ya watu wanaopata huduma za fedha ukilinganisha na asilimia 54.1 kwa Zanzibar. Asilimia 16.8, zaidi ya wastani wa Taifa, wanapata huduma za benki huko Kilimanjaro.
Mojawapo ya sababu za hali kuwa mbaya kwa Zanzibar ni taarifa kwamba wengi hawajishughulishi na uzalishaji.
Hii inaweza ikawa sababu ya wao kutopata huduma hizi kutokana na ukweli kwamba hawana uwezo wa kumudu gharama hizo.
Wakati Tanzania sasa ikiwa na matawi ya benki yanayofikia 50 kote nchini na watumiaji wa simu wapatao milioni 28, kuna haja ya watu wa visiwani kubadilika na kuondokana na mfumo huo wa maisha.
Mitandao ya simu iliyopo, bara ipo Zanzibar pia, jambo linalotoa fursa sawa kwa wote.
Licha ya kwamba ripoti hiyo inaonyesha watu wengi wanahifadhi fedha zao nyumbani, bado wanatuma na kupokea fedha kwa kutumia njia tofauti na hata kufanya malipo pia kwa njia hizo, mfano m-pesa, airtel money, tigo pesa na hata easy pesa.
Pamoja na sababu nyingi za Watanzania wengi kutotumia huduma hizi, bado kuna kila haja ya kubadilika na kutoishi kijima kwani uchumi wa nchi hii unakua na mwingiliano na mataifa mengine unaongezeka.
Kutokuwa na fedha za kutosha, umbali wa kufuata huduma na gharama kubwa za huduma hizo kumekuwa kukielezewa kuwa ni kikwazo kwa watu wengi kumudu huduma hizo wakati wa zoezi la ukusanyaji wa taarifa za utafiti huo.
Wakati taasisi za fedha zikishauriwa kuangalia gharama za huduma zao, wananchi hawana budi kubadilika ili kuendana na mfumo mpya wa dunia unaohamia ulimwengu wa malipo kwa njia ya mtandao (cashless economy). Kampuni ya simu nazo, kwa kuwa ni rahisi kutumia simu, ni vyema zikaiona fursa hii na kuitumia.
Elimu ya huduma hizo ni tatizo kubwa kwa wananchi wengi hasa tukizingatia kuwa theluthi moja ya Watanzania wote hawajui kusoma wala kuandika kama ilivyobainishwa hivi karibuni na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).
Kimsingi kuna kila sababu kwa Tanzania kuangalia namna gani inaweza kufanya ili kuharakisha maendeleo nchini hasa katika sekta hii ya fedha.
Chanzo:Mwananchi

MH:DADI FAKI DADI AITAKA WIZARA YA ELIMU PEMBA KUCHUKUA HATUA DHIDI YA WANAFUNZI WATORO MASHULENI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Zaidi ya wanafunzi 200 kati ya 363 wa shule ya Sekondari ya Msuka Wilaya ya Micheweni  Pemba hawahudhurii masomo  siku ya Ijumaa ya kila Wiki bila ya sababu za msingi .

Waalimu wa shule  hiyo wameyabainisha hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe Dadi Faki Dadi alipofanya ziara aya kuteembelea katika Shule hiyo .

Wamesema kuwa wanafunzi hao wamekuwa na kawaida ya kujipa mapumziko siku ya Ijumaa hali ambayo inachangia matokeo mabaya ya mitihani yao ya Taifa  ambapo wameiomba Serikali ya Mkoa kusaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa kitendo hicho .

Akizungumza  na walimu , wanafunzi pamoja na wajumbe wa kamati ya shule hiyo , Mkuu wa Mkoa ameiagiza Wizara ya Elimu Wilaya ya Micheweni kuchukua hatua za kinidhamu dhihdi ya wanafunzi  ambao wameifanya siku ya Ijumaa kuwa ni mapumziko yao .

Amesema kuwa Serikali haiwezi kuona sheria , kanuni na taratibu zinavunjwa hivyo ni lazima suala hilo likomeshwe mara moja ili kuejnga maadili mema kwa wanafunzi .

Afisa Elimu na Mafunzio ya Amali Wilaya ya Micheweni Mbwana Shaame Said amesema kuwa wamepanga kukutana na wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ili kutafuta njia ya kukabiliana na tatizo hilo .

KAULI 7 ZA MAALIM SEIF KUHUSU MUUNGANO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

MAALIM
Amekua mmiliki wa vichwa vya habari kutokana na ripoti mbalimbali ambazo zimekua zikimnukuu kwa kudai kutozitaka serikali mbili lakini leo April 15 2014 amezungumza kwenye maonyesho ya miaka 50 ya muungano ya kuzitoa hizi kauli zifuatazo.


1. ‘Pamoja na milima na mabonde, muungano huu umedumu miaka 50, nchi nyingine zilishindwa, lazima tufanye tathmini hasa ya muungano wetu, lazima vijana waelimishwe vp muungano uliundwa, tulianzia vipi’
2.‘Ukitaka upate maenedeleo, yatambue mafanikio yako lakini pia usisahau matatizo yako, ni ni moja.. kufanya vizuri, Sidhani katika Tanzania kama kuna watu hawataki muungano, na kama wapo ni wachache, muungano uendelee ndio la msingi’


3. ‘Sio dhambi watu kuwa na fikra tofauti, sio dhambi hata kidogo kwa sababu hatuwezi wote kuwa na fikra aina moja, Wanaotaka serikali moja wasibezwe, mbili wasibezwe, wanaotaka tatu na serikali ya mkataba wasikilizwe pia’
4. ‘Wako wanaoamini kwamba matatizo ya muungano yako kwenye muundo, tuwasikilize wana hoja gani, Mwaka 1963 Malaysia na Tanganyika maendeleo ya sehemu zote hizi yalikua sawa, mwaka 2014 tujiulize, changamoto kwetu ni vipi tutakua na muungano utakaokua ni chachu ya maendeleo ya haraka, mambo ya 74 ni tofauti na 2014′
5. ‘Tuwe makini sana, sote ni wa nchi moja, tujiepushe na kikundi chochote kuona wao wana haki zaidi, Watanzania wote sawa, wajumbe wa bunge maalum waangalie maslahi ya nchi, muungano huu ni wa nchi 2 zilizokua dola huru na kuungana kwa hiari’
6. ‘Tupate katiba ambayo itaondoa migogoro, kero iwe ni historia… hili swala lisiwepo tena, tusiende kwenye maamuzi ya harahaharaka tukasema serikali mbili au tatu bila kuangalia athari zake, katiba ya Znz inasema ni miongoni mwa nchi mbili za muungano, ya Muungano inasema Tz ni nchi moja, huo ni mgogoro’
7. ‘Nadhani Warioba walivyopendekezwa waliona hisia za Znz zilivyo, tunataka katiba itakayotambua usawa wa nchi mbili, hakuwezi kuwa na katiba ambayo itamridhisha kila mtu lakini angalau wengi wao waridhike’

MAWAZIRI ZANZIBAR WALIPULIWA BUNGENI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,Ismail Jussa Ladhu.
 
Mjumbe  wa Bunge Maalumu la Katiba, Ismail Jussa Ladhu, amewalipua mawaziri watatu wa Zanzibar kuwa ni ‘wanafiki’ kutokana na kushindwa kusimamia msimamo wao kuhusiana na Muungano.
Jussa alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiwasilisha maoni ya wajumbe wachache wa Kamati Namba Sita kuhusu Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba.

Aliwataja baadhi ya mawaziri, ambao walionyesha msimamo wao wakiwa Zanzibar na  baada ya kufika Dodoma wamegeuka, kuwa ni pamoja na Waziri wa Fedha, Yusuph Omary Mzee; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Utawala Bora), Mwinyi Haji Makame na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Kazi), Haroun Ally Suleiman.
Jussa alisema mawaziri hao wote walikuwa wakionyesha kukasirishwa na jinsi Muungano huo ulivyoisababishia Zanzibar kukwama kiuchumi.

“Mheshimiwa mwenyekiti, kuna rekodi hata na CD ya semina ya Baraza la Wawakilishi lililoitishwa na Mheshimiwa Spika wetu, Ameir Pandu Kificho…nashukuru sana Spika wetu, mawaziri watatu walionyesha ni jinsi gani wamedhalilishwa na Muunganoo huu. Lleo kimewapata nini Dodoma? Mimi sijui,” alisema Jussa.

Alisema kuna siku walikuwa wanajadili muswada wa kurekebisha sheria na kwamba, alipendekeza neno moja kwa njia ya maandishi ili kutoa kipaumbele cha ajira kwenye sekta ya utalii upande wa Muungano kisiwapo ila kiwapo kwa Zanzibar kwa kuwa ndiyo sekta ya utalii ilipo.

“Tukakataliwa. Mimi na Mheshimiwa Asha Bakari tulitoka naye nje ya Baraza la Wawakilishi, huku Asha akisema wenzie wamempinga. Lakini wamekuja Dodoma wamegeuka misimamo yao,” alisema Jussa.

Aliongeza: “Leo sisi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi…ambao tumesimama mara nyingi na Baraza la Wawakilishi kupigania Muungano kutoka pande zote mbili (CCM na CUF) kulalamikia…leo tumefika Dodoma, wengine wamefyata.”

Alisema Wazanzibar wengi hawaridhishwi na muundo uliopo sasa wa Muungano kwa kuwa umekuwa ukiwanyonya zaidi na kuwapendelea Watanganyika.

Jussa alisema katika mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yapo mambo 17 ya ushirikiano, lakini katika hayo, mambo manne tu ndiyo ya Jamhuri ya Muungano.

Aliyataja mambo hayo, ambayo wana ushirikiano na Jamhuri ya Muungano kuwa ni ushirikiano katika mambo ya fedha na uchumi, haki ya ukazi, ushirikiano katika mambo ya siasa, uhuru wa mtu kwenda atakapo na uhuru wa kazi.

Kuhusu upotoshaji kwamba, kuruhusu serikali tatu ni kuvunja Muungano na kumrejesha Sultani, Jussa alisema Januari 12, 2000 katika Uwanja wa Amani mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Benjamin Mkapa, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Salmin Amour, alitoa msamaha na kumwambia Sultan kuwa anaweza kurudi Zanzibar.

“Je, alipokuwa anatoa msamaha huo, alikuwa anakiwakilisha chama gain? na kusema akifika serikali itampa kila aina ya msaada na arudi kuwa raia wa Zanzibar…mheshimiwa mwenyekiti kwa zana hii tunajua basi kama kuna watu, ambao wanataka kurejesha mambo ya Sultani basi kitakuwa ni Chama Cha Mapinduzi kwa kutumia kauli hii, ambayo haikufutwa hadi hii leo,” alisema.

Alisema ikiwa kila anayedai serikali tatu anataka kumresheja Sultani. “Najiuliza je, katika waasisi wa Afro Shiraz aliyekuwa katibu mipango badala ya Rais wa Afro Shiraz, Mzee Jumbe alipotaka serikali tatu…alikuwa na nia ya kumrejesha Sultan?” alihoji

Jussa alisema utaratibu wa kila siku kuzusha mzuka wa Sultani ili kuzima hoja ya serikali tatu haitawasaidia kitu chochote.

“Kama hoja ni kwamba, Zanzibar iliwahi kutawaliwa na Sultani…mimi nilipokuja hapa (bungeni) katika maktaba yako nilipitia katiba ya Tanganyika ya Uhuru ya mwaka 1961…katiba ile bado ilikuwa inaendelea kumtambua Malkia kama ni mkuu wa nchi ya Tanganyika,” alisema.

Aliongeza: “Na ilikuwa na Gavana hapa, ambaye alikuwa na mamlaka kama aliyokuwa nayo Sultani…lakini hata siku moja Watanganyika wakitoa maoni yao hawaambiwi kwamba, wanataka kurudisha Malkia au Gavana wa Tanganyika.”

HATI HALISI YA MUUNGANO KUWASILISHWA BUNGENI

Baada ya madai ya muda mrefu ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu ya Katiba kutaka hati halisi ya makubaliano Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iwasilishwe bungeni ili kuthibitisha uhalali wake, hatimaye serikali imeahidi kuwasilisha hati hiyo bungeni.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, kabla ya kuwasilisha maoni ya wajumbe wa kamati Namba Sita juu ya sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya katiba.

Wasira alisema hayo baada ya awali mjumbe wa Bunge hilo, Tundu Lissu, wakati akitoa ufafanuzi wa maoni ya wachache wa kamati namba nne kuhusiana na sura hizo, kudai kuwa hati za Muungano hazipo mahali popote, hivyo Muungano uliopo siyo halali.

Alisema hati hiyo ipo na imehifadhiwa katika hali nzuri, hivyo itawasilishwa bungeni ndani ya siku mbili zijazo.

Kauli hiyo ya Wasira ilipokelewa kwa vifijo na wajumbe wa Bunge hilo bila ya kujali tofauti zao.

“Naahidi kwa niaba ya dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa hati ipo na itawasilishwa hapa ndani ya siku mbili zijazo na ina sahihi za waasisi wetu, hayati Mwalimu Julius Nyerere, na marehemu Abeid Amani Karume,” alisema Wasira.

Kauli ya Wassira ilikuja baada ya kuwapo kwa utata juu ya hati hiyo, kwani wajumbe wengi wakati wakijadili sura za rasimu hiyo katika kamati zao, walihoji uhalali wa hati hiyo na sehemu ilipo.

Kumekuwa na madai kuwa hati hiyo ipo Umoja wa Mataifa (UN), huku taarifa nyingine ikisema ipo katika Ikulu ya Dar es Salaam na Zanzibar, ambako zimehifadhiwa baada ya Nyerere na Hayati Karume kutia saini na kubadilishana.

Pia baadhi ya wajumbe wa kamati hizo, walikuwa wakihoji sahihi za aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Nyerere na aliyekuwa Rais wa Serikali ya Watu wa Zanzibar, Karume wakidai kuwa zimeghushiwa.
 
MNYIKA ASHUPALIA HATI
Pamoja na maelezo hayo ya Wasira, Mjumbe John Mnyika, aliendeleza hoja ya kutaka kuona hati halisi za makubalino ya Muungano kabla ya kuanza mjadala wa kuchambua sura hizo za rasimu ya katiba.

Akiongea kwa jazba, Mnyika alimkumbusha Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kuwa amemuandikia barua akiomba Bunge hilo liahirishwe hadi hapo hati halisi zitakapowasilishwa bungeni ili wathibitishe uhalali wake.

“Leo nimekuandikia barua rasmi nisichangie lolote hadi hati ziwasilishwe au Bunge lisianze mjadala hadi hati ziwasilishwe kwanza. Maana isijekuwa Wasira ametuuzia mbuzi kwenye gunia…” alisema Mnyika.

Akijibu ombi hilo, Sitta alisema: “Mwenye mamlaka ya kupanga shughuli za Bunge ni Kamati ya Uongozi na hili la Mnyika ni la ajabu. Eti kuwa asipoona hati sisi wote tuache kazi mpaka ipatikane. Haiwezekani. Na maombi ya namna hiyo hayakubaliki,” alisema Sitta.

Aliongeza: “Bunge hili linaendeshwa kwa gharama kubwa za wananchi. Na mambo kama hayo hayakubaliki na kuwaonya wanapoomba kitu wasimuwekee mwenyekiti bastola kichwani.”

Kwa upande wake, mjumbe mwingine, Freemaan Mbowe, alimpongeza Wasira kwa kuliahidi Bunge kuwa hati hizo zitawasilishwa bungeni ili wajumbe wazione.

Hata hivyo, aliomba hati hizo kuwasilishwa haraka badala ya kuchukua siku mbili, kwa kile alichosema zimeleta utata mkubwa na kuufanya mjadala mzima kukosa nguvu.

“Kwa umuhimu wa mjadala huu, serikali ina uwezo wa kuileta hati hata leo. Tunachoomba iletwe haraka, kwa sababu ndiyo msingi wa majadiliano. Uhalali wake tutaangalia itakapoletwa na kuiona,” alisema Mbowe.

MBOWE ATAKA BUNGE LIVUNJWE
Mjumbe Freeman Mbowe, ametaka Bunge hilo livunjiliwe mbali kama msingi wake wa serikali tatu haukubaliki.

Aidha, amewataka wajumbe wanaowakilisha mapendekezo ya wengi wasiwabeza wajumbe wa tume kwani ni viongozi waandamizi wa serikali wanaoongoza nchi.

Akianza na hoja kuvunja Bunge hilo, Mbowe alisema kama rasimu inapuuzwa na kulazimisha kufuata mapendekezo ya serikali mbili hakuna haja ya kuendelea kuijadili.

Anaungana na Juma Duni Haji, aliyetahadharisha kuwa iwapo rasimu ya katiba ya serikali tatu haitakiwi serikali irudi tena kwa wananchi kuwauliza wanataka muundo gani.

“Tunapuuza msingi wa rasimu, ambao umetuweka hapa leo ni bora hii isiwepo ili aiandaliwe rasimu nyingine ya serikali mbili ambayo haijapendekezwa na tume.”

KASHFA KWA TUME
Alipinga kuwakashifu viongozi walioandaa rasimu hiyo, Jaji Joseph Warioba, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, na Katibu Mkuu wa uliokuwa Muungano wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk. Salim Ahmed Salim.

Alitaja baadhi ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa ni watumishi wa umma, wakiwamo waandamizi kutoka Ikulu na Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Mbowe alisema viongozi hao ndiyo waliotafiti, kuchambua nyaraka na kusikiliza maoni ya umma na kuandaa ripoti inayokashifiwa.

Alisema wanapohukumiwa kuwa wamefanya kazi chafu ya kuchakachua takwimu, umma uelewe kuwa takwimu hizo zimetangenezwa na watumishi waandamizi wanaoongoza serikali.

 “Viongozi wanaohudumu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano na na ya SMZ,” alitahadharisha.

Aliongeza: “Mnapobeza taarifa ya tume ambayo ni ya viongozi wa serikali na chama tawala mjue kuwa mnaikana serikali yenu na kuwakana watu wenye dhamana ya kusimamia nchi.”

Akizungumzia gharama, alisema taifa limetumia kodi za wananchi kuendesha tume hiyo na kwa mujibu wa taarifa za Bunge, karibu Sh. bilioni 68 zimetumika kufanya utafiti, ambao walio wengi leo wanaukana.

KUPINGWA

Wakati akiwasilisha taarifa hiyo, Mbowe alionywa na Mjumbe Fahmi Dovutwa, kuwa asiwatishe wala kuwazuia wajumbe kusema wanaloamini.

Alisema wajumbe wasikosolewe wanapohoji tatizo lililofanywa na kiongozi aliyeshika mamlaka. Alitaka watu wavumiliane na wajumbe wakubali ukweli.

Mbowe akimjibu Dovutwa, alisema hayuko bungeni kutetea wala kulaumu, bali kuzungumza hoja.

 “Warioba akikosea ama hayati Mwalimu Julius Nyerere watakosolewa. Lakini wakiwa na jambo jema wasifiwe,” alisema.

KIGWANGALLA AMTUHUMU SITTA
Wakati hayo yakijiri, hali ya kutoaminiana iliendelea kutawala katika Bunge hilo, baada ya Mjumbe Dk. Hamis Kigwangalla, kumtuhumu Sitta kuwa anapendelea upande wa wachache.

Dk. Kigwangalla alitoa tuhuma hizo bungeni jana baada ya kuomba utaratibu mara baada ya Sitta kumuita mjumbe wa kamati namba nne, Tundu Lissu, kumalizia muda uliobaki Ijumaa iliyopita kutokana na Bunge kuahirishwa kabla ya muda wake wakati akitoa ufafanuzi wa taarifa ya wachache ya kamati yake.

 Sitta aliahirisha Bunge hadi jana kutokana na kukatika ghafla kwa matangazo ya moja kwa moja ya Kituo cha Televisheni cha TBC wakati Lissu akitoa ufafanuzi huo.

Katika kikao cha jana, Sitta alimruhusu Lissu kumalizia kiporo cha muda uliobaki kabla ya kamati nyingine zilizokuwa zimesalia kusoma taarifa zao kuhusiana na sura ya kwanza na ya sita za rasimu ya katiba.

“Kama mnavyokumbuka Ijumaa tuliahirisha Bunge wakati Lissu akiendelea na kutoa utetezi wa wachache kwenye kamati yake kutokana na matatizo yaliyotokea TBC. Sasa namruhusu aje amalizie dakika 16 zilizokuwa zimebaki ili tuendelee na mambo mengine,” alisema Sitta.

Wakati Lissu akielekea katika sehemu maalumu ya mzungumzaji, Dk. Kigwangalla alisimama na kuomba utaratibu, akitaka na yeye apewe muda wa kusoma taarifa ya wachache, kwa maelezo kuwa amepata taarifa kuwa matangazo ya TBC yalikatikia wakati na yeye akiendelea kusoma taarifa ya wengi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti ili haki itendeke na mimi naomba nipewe nafasi ya kusoma taarifa ya wengi, nimepata taaarifa kuwa mitambo ya TBC ilizimika wakati na mimi nikisoma taarifa, Sababu gani Lissu apewe nafasi na mimi nisipewe,” alisema.

 Aliongeza: “Lakini Mwenyekiti umekuwa ukisikiliza zaidi upande wa wachache, unawapendelea, mimi siridhishwi na upendeleo huu.”

 Alidai muda uliokuwa umebaki kwa Lissu kumaliza kutoa ufafanuzi ulikuwa ni dakika mbili, lakini Sitta alimpa dakika 16.

 Akijibu taarifa hiyo, Sitta, alisema: “Nimesikitika kutuhumiwa kuwa nawapendelea wachache. Mimi nategemea wataalamu makatibu wangu hapa ambao wameniambia kuwa muda uliobaki ni dakika 16 na si dakika mbili. Lakini kama kuna mtu anahisi ninapendelea alete malalamiko kimaandishi kwa mujibu wa kanuni yatashughulikiwa.”

 Kuhusu madai ya  Dk. Kigwangalla kutaka na yeye apewe muda wa kusoma taarifa ya wachache, Sitta, alisema wakati matangazo ya TBC yalipokatika Lissu akitoa ufafanuzi wa taarifa ya wachache, kuna mjumbe alisimama na kuomba muongozo juu ya suala hilo, lakini kwa upande wa Kigwangalla hakupewa taarifa yoyote kuwa kulikuwa na tatizo hilo.

Pia alisema uchunguzi uliofanywa haujathibitisha kama ni kweli kuwa matangazo yalikatika wakati Dk. Kigwangalla akisoma taarifa ya wengi hivyo hawezi kutoa taarifa hiyo.

Hata hivyo, Sitta, aliwatahadharisha wajumbe kuwa kutokana na hali ya hewa kutotabirika, hasa katika mikoa ya Pwani, ambako mvua kubwa zinanyesha, mitambo ya televisheni ikizimika Bunge halitaahirishwa tena.

LISSU
Lissu jana aliendelea na madai yake yake kuwa hati za makubaliano ya Muungano hazipo mahali popote, hivyo Muungano uliopo siyo halali.

Alidai Mwasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliivunja Tanganyika na kuungana na Zanzibar kuwa Jamhuri ya Tanzania kwa amri (Presidential Decree) badala ya makubaliano ya pande mbili.

Imeandikwa na  Theodatus Muchunguzi, Abdallah Bawazir, Gaudensia Mngumi na Jacqueline Massano, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

MRADI WA ACRA KUNUFAISHA WAZANZIBZRI 15,000

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
ZAIDI ya watu 15,000 watafaidika na mradi wa pamoja baina ya Jumuiya ya Hifadhi ya Mji Mkongwe na Jumuiya ya ACRA utakaoanza hivi karibuni ili kuendeleza Mji Mkongwe.
 Hayo yalibainishwa na Mohammed Balow, Mwenyekiti wa Jumuiya ya uhifadhi Mji Mkongwe (Zanzibar Stone Town Heritage Society) katika hafla ya kutiliana saini kati yake na Nicola Moganti ambaye ni Mratibu wa Shirika la Maendeleo la ACRA.
 Miongoni mwa  watakaofaidika ni Wazanzibari, mafundi ujenzi 400, watu 75 wasio na ujuzi, wajasiriamali wa sekta ya ujenzi na ambao wamesajiliwa na jumuiya hiyo.
 Mradi huo utaanzisha maabara katika Chuo Kikuu cha SUZA ambapo utasaidia kufanya utafiti unaohusu malighafi zinazotumika kujenga majengo ya kihistoria. 
Mradi huo pia utasaidia kuandikwa kwa mtaala unaohusu kufanya matengenezo ya majengo ya kale ambao mtaala huo utatumiwa na Chuo cha Karume (Karume Institute of Science and Technology) na kufanya mikutano na wadau mbalimbali kuzungumzia masuala ya urithi na utamaduni yakiwemo majengo ya kiasili yaliyopo Zanzibar.
 Jumuiya ya uhifadhi Mji Kongwe ndio itakayokuwa muhusika mkuu katika kupanga na kutekeleza shughuli zinazohusu kutoa taaluma na kukuza uelewa wa masuala ya kihistoria na urithi wa utamaduni uliopo visiwani humo huku ikiandaa na kufanya kampeni kwa skuli zenye lengo la kutoa taaluma kwa ajili ya kukuza uelewa juu ya masuala ya urithi na utamaduni wa Zanzibar. 
Mradi huo wa miaka mitatu wenye lengo la kuhifadhi na kutunza urithi wa utamaduni Zanzibar na kuhifadhi sekta hii kwa kuchangia ukuaji wa uchumi nchini utagharimu jumla ya EURO 1,200,000.
Chanzo:Tanzania Daima

WAASISI ZANZIBAR WATOA YA MOYONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKE wa marehemu Abeid Amaan Karume, Mama Fatma Karume aliwataka vijana kuyaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa kuacha chuki za ukabila, kidini ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliyasema hayo katika Hitma ya Hayati Karume aliyeuawa kikatili Aprili 7 mwaka 1972 katika jengo la Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui pamoja na viongozi wengine wa chama cha ASP.
Katika mashambulio hayo aliyekuwa Katibu Mkuu wa ASP Shekhe Thabit Kombo alijeruhiwa kwa kupigwa risasi ya mguu.
“Vijana tuachane na chuki za ukabila na za kidini ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko wa wananchi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania....tuishi kama walivyotuagiza wazee wetu,” alisema.
Hitma hiyo iliongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Shekhe Khamis Haji na kuhudhuriwa na viongozi wa kidini na serikali, akiwemo Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Katika maelezo yake, Mama Fatma alisihi vijana kuishi kama alivyofikiria muasisi huyo wa mapinduzi ya Zanzibar ya kutokuwepo kwa ubaguzi wa aina yoyote ile.
Alisema ukombozi wa nchi ya Zanzibar umeletwa na Mapinduzi ambapo kabla ya hapo hakuna mwananchi aliyekuwa na uwezo wa kumiliki ardhi kwa ajili ya kujenga nyumba au shughuli za Kilimo.
“Tunapomkumbuka hayati Karume basi tunatakiwa kuyaenzi yale mambo yote mema ambayo yeye aliyasimamia kwa kipindi chote cha uhai wake,” alisema Mama Fatma.
Alisema Karume alichukia chuki na ukabila zilizowabagua Waafrika katika nchi yao, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliyosababisha kufanyika kwa Mapinduzi ya mwaka 1964.
Naye mmoja wa viongozi wa waasisi walioshiriki katika Mapinduzi ya mwaka 1964, Mzee Juma Ame (88) alisema utu wa Mwafrika ulikuwa huru kutokana na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyoongozwa na Karume.
Ame, ambaye alipata kushika nyadhifa mbalimbali katika Chama cha ASP hadi Chama Cha Mapinduzi, alisema Karume mara baada ya kushika hatamu ya kuongoza dola, alitekeleza manifesto ya chama cha ASP ambayo iliweka kipaumbele suala la wazalendo kumiliki ardhi ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi.
“Karume alitekeleza manifesto ya ASP kwa kugawa ardhi eka tatu tatu kwa wananchi wa Unguja na Pemba kwa ajili ya kazi za kilimo na ujenzi wa nyumba katika mwaka 1965,” alisema.
Naye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Makame Mzee aliwataka Wazanzibari kuyaenzi yale mambo yote muhimu yaliyoasisiwa na Karume ambayo yameleta manufaa makubwa wa Wazanzibari, ikiwemo Muungano.
“Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo mambo makuu ambayo Karume aliyapa kipaumbele..... tulipofanya Mapinduzi mwaka 1964 tulikaa muda wa miezi minne tu tukaungana na wenzetu wa Tanzania Bara na kuzaliwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano,” alisema Mzee.
Katika kisomo cha hitma kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano, Alhaji Ali Hassan Mwinyi pamoja na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Aidha katika kisomo cha hitma kilichohudhuriwa pia na wanawake akiwemo mjane wa marehemu mama Fatma Karume, wake wa viongozi wakuu pamoja na wajukuu wa marehemu.
Wakati huo huo, vijana wa Chama Cha Mapinduzi wametakiwa kumuenzi rais wa kwanza wa Zanzibar Abeid Amaan Karume kwa kufanya kazi na kuweka maslahi ya taifa mbele.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Khamis Juma wakati akifunga kongamano la vijana wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu wajibu wao na kumuenzi hayati Karume.
Alisema miongoni mwa taasisi ambazo zilipewa kipaumbele cha kwanza na Karume ni Umoja wa Vijana wa ASP, ambapo aliamini kwamba vijana ndiyo nguvu za chama imara watakaojenga taifa.
Aidha, Sadifa aliwataka vijana kamwe kuacha kuyumbishwa na watu mbali mbali wasioitakia mema Zanzibar pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni kielelezo cha taifa.
Alisema miongoni mwa mambo ambayo yalipewa kipaumbele na Karume ni kuziunganisha nchi mbili zilizokuwa huru na kuzaliwa kwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, mwaka 1964.
Alisema faida za Muungano zinaonekana hii leo ambapo wananchi wa Zanzibar wapo huru kuishi sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupiga hatua kubwa za maendeleo na uchumi.
“Tunapomkumbuka hayati Karume basi tunatakiwa pia kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni matokeo ya juhudi binafsi za mwasisi wa taifa hili,”alisema.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unatimiza umri wa miaka 50 ifikapo Aprili 26 mwaka huu, ukiwa Muungano wa kupigiwa mfano ulioweza kudumu duniani hadi sasa.
Kongamano la kumuenzi hayati Karume lilitayarishwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na ofisi ya mkoa wa Mjini Magharibi ya chama hicho.
Katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ameongoza wananchi mbali mbali katika hitma ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume iliyofanyika katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa.
Aidha viongozi wakuu wa nchi waliweka shada la maua pamoja na wanafamilia wa marehemu na waliokuwa waasisi wa mapinduzi walioshirikiana na marehemu.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliweka shada la maua katika kaburi la marehemu lililopo pembeni mwa jengo la Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Aidha Rais Kikwete aliweka shada la maua katika kaburi la marehemu ambaye hadi anauawa alikuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kiongozi aliyeshiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar, Juma Ame naye aliweka shada la maua katika kaburi la marehemu kwa niaba ya wazee walioshiriki katika Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964.
 Chanzo;Habari Leo
 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa